MARIA; Kuzaliwa kwa Yesu ni mwanzo wa Agano Jipya na la milele
na ni kilele cha ahadi ya Mungu kwa Daudi mtumishi wake. Mfalme Daudi
ambaye Yesu amezaliwa katika ukoo wake, anakumbukwa daima na wana wa
Israeli kwa sababu alilifanya taifa hilo kuwa imara na lenye nguvu kati
ya mataifa mengine. Lakini hasa, mfalme Daudi anakumbukwa sana
katika Historia ya Ukombozi kwa sababu yeye ndiye pekee aliyelienzi
sanduku la agano kwa kulihamishia mjini Yerusalemu na kuamuru hekalu
lijengwe. Sanduku la Agano la Kale lilitengenezwa kwa mbao na kupambwa
kwa dhahabu. Ndani ya sanduku hilo kuliwekwa mawe mawili yenye kuandikwa
Amri za Mungu juu yake. Wana wa Israeli walizitambua Amri za Mungu kuwa
ni Neno la Mungu na wakalihifadhi ndani ya sanduku kwa heshima na
uchaji mkubwa. Sanduku hilo likawa ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati
yao. Ili kuonesha heshima kubwa zaidi, wana wa Israeli walijenga hekalu
ambalo ndani yake kulitengwa chumba cha kuhifadhia Sanduku la Agano.
Chumba hicho kilichoitwa patakatifu pa patakatifu. Sura ya Nne Sanduku
la Agano Jipya Mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo
tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye
hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya
nyama. 2 Wakorintho 3:3 Tangu awali Kanisa linafundisha kuwa Mungu
anafanya agano jipya na watu wake kwa kuongea na mioyo yao. Katika agano
la kale Mungu aliongea na watu wake kwa njia ya Musa. Mtume Paulo
anathibitisha tofauti kati ya agano la awali kwa njia ya Musa na agano
la sasa kwa njia ya Yesu Kristo. Katika agano la awali Mungu aliandika
Neno lake juu ya mbao mbili za mawe ambazo wana wa Israeli
walidhihifadhi ndani ya sanduku la mbao lilipambwa kwa dhahabu. Katika
agano la sasa Mungu ameandika Neno lake ndani ya moyo wa kila amwaminiye
Kristo. Utabiri wa kufanyika kwa agano jipya na kuandikwa kwa Neno la
Mungu ndani ya moyo wa mwanadamu ulifanywa na nabii Yeremia na nabii
Ezekieli miaka mingi kabla ya Kristo: Bali agano hili ndilo
nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana:
Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika. Nami
nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Yeremia 31:33 Nami nitawapa
moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa
kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama, ili waende katika
amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu
wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Ezekieli 11:19-20 Utabiri wa nabii
Yeremia na Ezekieli ulitimia kwa Yesu Kristo, mwana wa Maria. Yesu
Kristo ndiye Neno wa Mungu aliyekuja duniani na kuweka makao yake ndani
ya mioyo ya watu wamwaminio. Katika Agano la Kale lililofanyika kwa njia
ya Musa; Neno la Mungu liliandikwa juu ya mawe mawili na kuhifadhiwa
ndani ya Sanduku la Agano. Katika Agano Jipya lililofanyika kwa njia ya
Yesu Kristo; Neno la Mungu linaandikwa ndani ya mioyo ya wote waamini na
sio tena juu ya mawe. Neno la Mungu ni Yesu mwenyewe na kila aaminiye
na kumpokea anafanywa kuwa ni Sanduku la Agano Jipya: Hapo mwanzo
kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala
pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika……. Wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina
lake; waliozaliwa si kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa
mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa
kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye
kwa Baba; amejaa neema na kweli……… Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi
sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa
mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Yohane
1:1-3, 12-14, 16-17 Bikira Maria ndiye wa kwanza kuwa ni Sanduku la
Agano Jipya. Nyakati za utabiri wa manabii zilipotimia, Mungu alimtuma
malaika Gabrieli kwa Bikira Maria ili kumpasha habari ya kuteuliwa kwake
kuwa ni mama wa mkombozi. Bikira Maria aliamini, akaukubali uteuzi huo
mtakatifu na akampokea Neno wa Mungu katika moyo wake na huyo Neno
akafanyika mwili ndani ya mwili wa Bikira Maria na sisi tukampata
mkombozi: Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu: Mwezi wa sita,
malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina
lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina
lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi; jina lake bikira huyo ni Maria. Akaingia
nyumbani kwake akasema, “Salamu uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.”
Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni: salamu
hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, kwa maana
umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukuwa mimba na kuzaa mtoto
mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana
wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna
mwisho. Maria akamwambia malaika, “Litakuwaje neno hili, maana sijui
mume? Malaika akajibu akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako,
na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena tazama, jamaa
yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake;
na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno
lisilowezekana kwa Mungu. Maria akasema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa
Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akaenda
zake. Luka 1:26-38 Mimba ya Bikira Maria ilikuwa ni Neno la Mungu
lililofanyika mwili ili likae pamoja nasi. Neno hilo ndani ya tumbo lake
linamfanya Bikira Maria awe ni Sanduku la Agano Jipya kwa kuwa
alisadiki na akajazwa neema toka kwa Mungu. Elizabeti ndiye
aliyethibitisha kuwa Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya. Wakati huo,
Elizabeti pia alikuwa ana mimba: Basi, Maria akaondoka siku hizo,
akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,
akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti. Ikawa Elizabeti
aliposikia kule kuamkia kwake Maria, kitoto kichanga kikaruka ndani ya
tumbo lake; Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu
akasema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie
mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto
kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri
aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana…… Maria akakaa
naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake. Luka
1:39-45, 56 Itaendelea