MAKANISA mawili katika Jimbo Katoliki Same yametabarukiwa katika
nyakati tofauti na Balozi wa Papa hapa nchini pamoja na askofu wa Jimbo
hilo Rogath Kimaryo. Makanisa hayo ni Kanisa la Mtakatifu
Yoseph Mfanyakazi kigango cha Lomwe katika parokia ya Mtakatifu Yuda
Thadei Usangi lililotabarukiwa na Askofu Mkuu Fransisko Padilla, na
Kanisa la Familia Takatifu Parokia ya Lembeni lililotabarukiwa na Askofu
Rogath Kimaryo CSSP wa Jimbo Katoliki Same akishirikiana na Askofu Paul
Semugerere wa Uganda. Balozi wa Vatikani nchini Askofu Mkuu Fransisko
Padilla amepokelewa kwa shangwe na mwenyeji wake Askofu Rogath Kimaryo
wa Jimbo Katoliki Same pamoja na waamini wakiwepo mapadri, watawa na
waamini walei. Akitabaruku Kanisa la Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi kigango
cha Lomwe katika parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Usangi jimboni humo,
Askofu Mkuu Padilla amewaasa waamini watambue wajibu wao kutegemeza
Kanisa pamoja na paroko wao. “Mtambue kuwa, Kanisa la Mungu hapa Lomwe
lina watu wenye uwezo mbalimbali wakimwemo wakulima, waajiriwa,
wafanyabiashara ndogondogo na wafugaji. Hivyo lazima kujenga muungano wa
sisi kwa sisi ili kusambaza injili ya Kristo katika eneo hili,” amesema
Askofu Mkuu Padilla. Amesisitiza kujenga parokia katika msingi wa imani
na hivyo kuwapokea wahitaji wa aina mbalimbali kiroho na kimwili. Aidha
amesisitiza wanakanisa kusali na kuonesha matendo ya huruma kwa watu
wote. Amewataka wajisikie furaha kulea miito ili siku moja kuwepo padri
na watawa kutoka katika kigango hicho ili kushusha nyavu kuvua pamoja na
Yesu. Amewataka waamini wajenge juhudi katika kuvua si wale tu
wasiofahamu bali pia na wale walegevu na hivyo kuonesha sura ya Kristo
kwa watu wote. “Tuogope kujihubiri wenyewe bali kumhubiri Kristo
aliyekufa na kufufuka.” Balozi Padilla amekazia. Ameongeza “Ni vema
kutafuta kondoo waliopotea tukiwapenda wote na kuwalinda huku tukiwapa
tumaini la daima.” Askofu Mkuu Padilla amesisitiza kuwa jengo hilo liwe
kweli nyumba ya sala na majadiliano ya kiroho. “Kwa kufungua na kubariki
jengo hili basi mioyo ifunguliwe na kuguswa na Mungu. Kwa njia hiyo
kuwepo mahusiano na masikilizano tukijua kuwa sote tu familia moja ya
Mungu.” Ametoa mwito kwa wakristo kuwa na tabia ya kukubali mawazo ya
wengine ili kuimarisha si idadi ya watu bali nguvu ya imani. Ili
kufanikisha hayo, amewataka wote kujenga moyo wa kurithisha imani kwa
watoto ili kuilinda na kuitetea kwa mapendo. Akistaajabu mandhari ya
Lomwe Usangi, Askofu Mkuu Padilla amesema Wakristo katika eneo hilo
lililopo katika milima ya upare wajivunie kwa vile wako juu karibu na
mawingu hivyo, wako karibu na Mungu na Baraka za Mungu huwafikia kwa
haraka. Wakati wa kutabaruku Kanisa hilo, Askofu Mkuu Padilla alibatiza
watoto kumi waliokuwa wameandaliwa kama ishara maalum kwa utume wa
Kristo wa kuwabatiza na kuwafundisha. Aidha ameongoza misa takatifu
katika Kanisa Kuu la Kristo Mchungaji Mwema Same ambapo alitoa
sakramenti ya kipaimara kwa waamini mia moja na ishirini na tano, na
baadaye kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya mapadri na kubariki Groto
ya Bikira Maria iliyopo katika uwanja wa Kanisa Kuu la Jimbo hilo. Pia
ametembelea Parokia mama ya Jimbo ambayo ni Parokia ya Kilomeni na
kubariki kikanisa cha masista. Hapo amewaasa wafurahi kwani kuwa juu ya
milima ni kuwa karibu na mbingu na karibu na Mungu hivyo hupokea Baraka
za Mungu kabla ya wengine. Katika adhimisho hilo walihudhuria pia Waziri
Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya (Baba wa Mwanga), Mkuu wa Wilaya ya
Same Herman Kapufi na wageni wengine kutoka madhehebu mbalimbali ya
Kikristo na serikali. Uongozi wa parokia umewashukuru wafadhili
mbalimbali walioshiriki kujenga Kanisa hilo akiwemo Askofu Rogath
Kimaryo, Paroko wa parokia hiyo Wilehard Mduma, Bw. Lameki Mlacha, Bw.
Cassian Njowoka na wengine. Pia umewashukuru waliotoa eneo kwa uwanja wa
Kanisa na pia kwa barabara ya kufika kanisani. Kutabaruku Kanisa
Parokia ya Lembeni Akitabaruku Kanisa la Familia Takatifu Parokia ya
Lembeni Jimboni Same, Askofu Rogath Kimaryo CSSP ametoa wito kwa waamini
Wakatoliki kutunza majengo ya Kanisa ili yasiwe magofu bali kuonesha
heshima ya pekee kwa Mungu ndani ya hekalu lake. “Tutunze nyumba ya Baba
wala tusiichezee isije ikageuka gofu kwani kama tukiwa sisi tu wachovu
wa imani jengo hili litakuwa kama gofu. Tusijaribu kupingana na hekalu
la Bwana, yaani tusiwe kinyume, tusipinge Kanisa na daima tutambue kuwa
Yesu ndiye silaha yetu. Sisi kama alivyokuwa Yesu tuwe na wivu na nyumba
ya Baba,” amesema Askofu Rogath. Ameendelea, “Kutabaruku Kanisa hili
kulete nguvu kwa njia ya Baraka ya Kanisa hili na tukwepe kuruhusu
wachungaji wanaopitia madirishani, tuwakaribishe wote kwani wanapofika
hawatarudi mikono mitupu kwani ni nyumba ya Mungu.” Amesisitiza kuwa,
waamini ndiyo hekalu la Mungu yaani mawe yaliyo hai, hekalu la kweli na
jiwe hai ambalo lilikataliwa na makandarasi lakini likawa jiwe kuu la
pembeni. Kwa jinsi hiyo amewaasa wote walioshiriki waepukane na hali ya
kutafuta kuangukiwa na jiwe hilo au kujikwaa katika jiwe hilo maana
wakifanya hivyo hawatafaulu wala kupona. Aidha ameeleza jinsi waana wa
Israeli walivyokaa uhamishoni Babeli na walivyorudishwa kwao kwa uongozi
wa Nehemia aliyekuwa kiongozi aliyejaa unyenyekevu; na jinsi Nehemia
alivyowataka watu wamjengee Mungu nyumba ya kuabudia kama utambulisho
wao wakizingatia kuwa hekalu lilishabomolewa. Amesema kuwa siku hiyo ni
siku ya Wanalembeni kufurahi na kumshukuru Mungu kwa makuu
aliyowafanyia. Tusugue magoti yetu katika Kanisa hili kujiombea na
kuombea wafadhili wetu ili neema za Mungu ziendelee kumiminika ndani
mwetu. Askofu Rogath amewashukuru Mapadri hususani Paroko wa parokia
hiyo padri Vicent Ndemchilio, wafadhili mbalimbali akiwemo Waziri
Mstaafu Bw. Cleopa Msuya na Virani Mkomba kwa majitoleo yao ya kupenda
maendeleo, na mshikamano bila kujali dini au dhehebu. Bw. Virani
ameshirikisha yake ya moyoni akitanabaisha kuwa, kazi hiyo ilianza kwake
kama njozi ambayo alimshirikisha mke wake na wazazi wake. Kwa nia njema
wote waliafiki maono yake kuwa amjengee Mungu Kanisa. “Ieleweke kuwa
thamani ya kujenga Kanisa ni kubwa na imegharimu vingi na kwa vile ni
sadaka siyo majigambo itabaki siri moyo mwangu.” amesema Virani na
kuendelea kuwa, “Ninawashukuru wafanyakazi wa kampuni ya VIGU kwa
kufunga mkanda na kujitoa ili kufanikisha kazi hii ya kumpa Mungu
heshima.” Parokia hiyo imejenga Kanisa jipya kuanzia April 13, 2013 na
kutabarukiwa Mei 29, 2014, baada ya kuvunja Kanisa la zamani
lililojengwa 1970.
0 comments:
Post a Comment