MAKALA

Monday, June 9, 2014

Bikira Maria Sanduku la Agano Jipya


 BIKIRA
MARIA; Kuzaliwa kwa Yesu ni mwanzo wa Agano Jipya na la milele na ni kilele cha ahadi ya Mungu kwa Daudi mtumishi wake. Mfalme Daudi ambaye Yesu amezaliwa katika ukoo wake, anakumbukwa daima na wana wa Israeli kwa sababu alilifanya taifa hilo kuwa imara na lenye nguvu kati ya mataifa mengine. Lakini hasa, mfalme Daudi anakumbukwa sana katika Historia ya Ukombozi kwa sababu yeye ndiye pekee aliyelienzi sanduku la agano kwa kulihamishia mjini Yerusalemu na kuamuru hekalu lijengwe. Sanduku la Agano la Kale lilitengenezwa kwa mbao na kupambwa kwa dhahabu. Ndani ya sanduku hilo kuliwekwa mawe mawili yenye kuandikwa Amri za Mungu juu yake. Wana wa Israeli walizitambua Amri za Mungu kuwa ni Neno la Mungu na wakalihifadhi ndani ya sanduku kwa heshima na uchaji mkubwa. Sanduku hilo likawa ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati yao. Ili kuonesha heshima kubwa zaidi, wana wa Israeli walijenga hekalu ambalo ndani yake kulitengwa chumba cha kuhifadhia Sanduku la Agano. Chumba hicho kilichoitwa patakatifu pa patakatifu. Sura ya Nne Sanduku la Agano Jipya Mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama. 2 Wakorintho 3:3 Tangu awali Kanisa linafundisha kuwa Mungu anafanya agano jipya na watu wake kwa kuongea na mioyo yao. Katika agano la kale Mungu aliongea na watu wake kwa njia ya Musa. Mtume Paulo anathibitisha tofauti kati ya agano la awali kwa njia ya Musa na agano la sasa kwa njia ya Yesu Kristo. Katika agano la awali Mungu aliandika Neno lake juu ya mbao mbili za mawe ambazo wana wa Israeli walidhihifadhi ndani ya sanduku la mbao lilipambwa kwa dhahabu. Katika agano la sasa Mungu ameandika Neno lake ndani ya moyo wa kila amwaminiye Kristo. Utabiri wa kufanyika kwa agano jipya na kuandikwa kwa Neno la Mungu ndani ya moyo wa mwanadamu ulifanywa na nabii Yeremia na nabii Ezekieli miaka mingi kabla ya Kristo: Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana: Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika. Nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Yeremia 31:33 Nami nitawapa moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama, ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Ezekieli 11:19-20 Utabiri wa nabii Yeremia na Ezekieli ulitimia kwa Yesu Kristo, mwana wa Maria. Yesu Kristo ndiye Neno wa Mungu aliyekuja duniani na kuweka makao yake ndani ya mioyo ya watu wamwaminio. Katika Agano la Kale lililofanyika kwa njia ya Musa; Neno la Mungu liliandikwa juu ya mawe mawili na kuhifadhiwa ndani ya Sanduku la Agano. Katika Agano Jipya lililofanyika kwa njia ya Yesu Kristo; Neno la Mungu linaandikwa ndani ya mioyo ya wote waamini na sio tena juu ya mawe. Neno la Mungu ni Yesu mwenyewe na kila aaminiye na kumpokea anafanywa kuwa ni Sanduku la Agano Jipya: Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika……. Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa si kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli……… Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Yohane 1:1-3, 12-14, 16-17 Bikira Maria ndiye wa kwanza kuwa ni Sanduku la Agano Jipya. Nyakati za utabiri wa manabii zilipotimia, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa Bikira Maria ili kumpasha habari ya kuteuliwa kwake kuwa ni mama wa mkombozi. Bikira Maria aliamini, akaukubali uteuzi huo mtakatifu na akampokea Neno wa Mungu katika moyo wake na huyo Neno akafanyika mwili ndani ya mwili wa Bikira Maria na sisi tukampata mkombozi: Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu: Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi; jina lake bikira huyo ni Maria. Akaingia nyumbani kwake akasema, “Salamu uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.” Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni: salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukuwa mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Maria akamwambia malaika, “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena tazama, jamaa yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Maria akasema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akaenda zake. Luka 1:26-38 Mimba ya Bikira Maria ilikuwa ni Neno la Mungu lililofanyika mwili ili likae pamoja nasi. Neno hilo ndani ya tumbo lake linamfanya Bikira Maria awe ni Sanduku la Agano Jipya kwa kuwa alisadiki na akajazwa neema toka kwa Mungu. Elizabeti ndiye aliyethibitisha kuwa Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya. Wakati huo, Elizabeti pia alikuwa ana mimba: Basi, Maria akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti. Ikawa Elizabeti aliposikia kule kuamkia kwake Maria, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana…… Maria akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake. Luka 1:39-45, 56 Itaendelea

0 comments:

Post a Comment