MAKALA

Monday, June 9, 2014

Wajawazito wadhalilishwa Ruvuma

WANAWAKE wajawazito katika kijiji cha Likuyuseka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanadhalilishwa katika zahanati ya kijiji hicho kwa kujifungulia katika chumba ambacho kinatumika kutibu wagonjwa wa kawaida. Ingawa kijiji cha Likuyuseka kipo mpakani na mgodi wa madini ya urani uliopo ndani ya pori la akiba la Selous ambalo lilitangazwa na shirika la umoja wa mataifa la unesco mwaka 1980 kuwa ni urithi wa dunia, hakijafaidika na mradi huo kwa kujengewa hospitali ambayo inatoa huduma yenye viwango. Wakizungumza na kiongozi, akina mama hao wamesema zahanati hiyo haina chumba maalum kwa ajili ya kujifungulia, hivyo chumba cha kujifungulia ni mkabala na chumba cha wagonjwa wa kawaida hali ambayo inawadhalilisha wanawake wanaojifungua. “Kila kitu ambacho kinafanywa na muuguzi wakati anamsaidia mama mjamzito kujifungua, wagonjwa wengine wanasikia, hali hii inatudhalilisha sisi wanawake. Tunataka uongozi ujenge chumba maalum cha kujifungulia kwani wanawake wengine wanaona aibu kufika hospitalini kujifungua, badala yake wanajifungulia kwa wakunga wa jadi na kuhatarisha maisha yao,’’amesema Fatuma Rajabu. “Zahanati hiyo ina miundombinu mibaya kwani ukifika hapo unaona upande mmoja yupo daktari anayehudumia wagonjwa wa kawaida, upande wa pili muuguzi mkunga anayehangaika kuwahudumia akina mama wajawazito. Hivyo mwanamke akijifungua anasikika kwa wagonjwa wengine wakiwepo watoto, vijana na wanaume. hii ni aibu sana kwa mama anayejifungua ndiyo maana wengine hawaendi kujifungulia hapo,’’ameeleza Mariam Rashid. Mwenyekiti wa kijiji cha Likuyuseka Athuman Rupia amekiri zahanati ya kijiji hicho kukosa chumba maalum kwa ajili ya kujifungulia akina mama wajawazito hali ambayo imesababisha wajawazito kujifungulia sehemu ya chumba ambacho pia kinatoa huduma kwa wagonjwa wengine. “Akina mama wajawazito wanapata shida wakati wa kujifungua hali hiyo inaweza kuchangia kuongeza tatizo la uzazi usio salama kwa kuwa kuna taarifa kuwa baadhi yao hawafiki kujifungulia katika zahanati hiyo kwa sababu ya aibu. Wagonjwa wengine wanawasikia kitu ambacho kinawadhalilisha wajawazito. ndiyo maana katika hospitali nyingine kuna wodi maalumu ya wazazi ili kuboresha huduma hizo,” amesema. Hata hivyo hakuna utafiti ambao umefanyika kuzunguka katika vitongoji vya kijiji hicho ili kubaini idadi ya wanawake walioamua kujifungulia kwa wakunga wa jadi, lakini baadhi ya wanawake waliohojiwa wamedai kuwa kuna wanawake hawaendi kujifungulia katika zahanati hiyo kutokana na kuona aibu. Katika kukabiliana na hali hiyo mwenyekiti huyo amesema mwaka huu kijiji kimefyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kujifungulia wajawazito ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kulinda hadhi ya mwanamke ambaye ni nguzo ya familia katika jamii. Kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho Maulid Kapolo ameeleza kuwa licha ya kuwepo changamoto ya kutokuwepo chumba cha wazazi, tatizo la vifo vya mama na mtoto lipo lakini siyo kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kuna madaktari na wauguzi wa afya wa kutosha na dawa zinapatikana kwa wingi katika zahanati hiyo inayohudumia watu zaidi ya 7000 . Wilaya ya Namtumbo ina vituo 43 vya kutolea huduma za Afya. Kati ya hivyo, vituo vya afya ni sita, vinne vya serikali na viwili vya shirika la dini, zahanati 37 kati ya hizo zahanati 34 za serikali na tatu zinamilikiwa na dini. Taarifa ya idara ya afya ya halmashauri ya wilaya ya Namtumbo imeyataja malengo makuu ya uboreshaji wa huduma za afya kuwa ni kuongeza kiwango cha chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 90 hadi 95 ifikapo 2015. Kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano na vifo vya akina mama vinavyotokea wakati wa kujifungua. Katika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia hususani lengo la tano la kupunguza vifo vya wajawazito, takwimu za wizara ya afya zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia 21 kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai, kutoka vifo laki moja kati ya mwaka 2004/2005 hadi vifo 454 kwa kiwango hicho kati ya mwaka 2009/ 2010. Mganga mafawidhi katika hospitali ya rufaa mkoani Ruvuma Benedicto Ngaiza ameeleza mikakati ya kuboresha huduma katika hospitali hiyo kuwa ni kuongeza juhudi ya kuisaidia serikali ili kuzuia vifo vya wanawake ambavyo hutokea wakati wa kujifungua. Amesema licha ya juhudi kufanywa na serikali na wadau katika kupunguza vifo vya akina mama, bado takwimu zinaonyesha kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya na kwamba inatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha wanawake wote wanajifungua salama bila kifo kutokea. Wanawake 8,700 hufariki dunia kila mwaka nchini Tanzania kutokana na matatizo ya ujauzito na hasa wakati wa kujifungua. takwimu hizi zinaonesha takribani wanawake 24 hupoteza maisha kila siku huku ikikadiriwa kuwa mwanamke mmoja hufa kila baada ya saa moja. Hata hivyo sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana katika kila kata ambapo kila kijiji kinatakiwa kuwa na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya na wataalamu wenye taaluma. Vingi kati ya vifo hivi vingeweza kuzuilika kama huduma za dharura zingekuwepo katika vituo vya tiba wakati wa kujifungua. Huduma zenyewe ni kama vile chumba cha upasuaji na wataalamu wake, vifaa tiba na uwezekano wa kuongezewa damu. “Si sahihi mama mjamzito kufa wakati wa kujifungua au kupoteza uhai wake kwa kuleta kiumbe kingine duniani, hii haiwezi kukubalika. na inasikitisha zaidi pale maisha ya mama huyu yanapotea hata kwa mambo ambayo yanaweza kuzuilika,” amesema Rais Kikwete katika hotuba yake mbele ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon. Sera ya afya inaeleza wazi kuwa serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine yakiwemo mashirika mbalimbali itahakikisha inaboresha huduma za afya ili ziwe na mazingira mazuri na vifaa tiba. Hata hivyo sera hiyo inakwenda kinyume na hali halisi unapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hasa vijijini mazingira siyo rafiki. Mazingira ya zahanati ya kijiji cha Likuyuseka yanafanana na mazingira mabovu ya kutolea huduma ya mama na mtoto katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na hata hospitali za rufaa katika nchi nzima.

0 comments:

Post a Comment