MAKALA

Monday, June 9, 2014

Balozi wa Papa nchini afanya utume Same

MAKANISA mawili katika Jimbo Katoliki Same yametabarukiwa katika nyakati tofauti na Balozi wa Papa hapa nchini pamoja na askofu wa Jimbo hilo Rogath Kimaryo. Makanisa hayo ni Kanisa la Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi kigango cha Lomwe katika parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Usangi lililotabarukiwa na Askofu Mkuu Fransisko Padilla, na Kanisa la Familia Takatifu Parokia ya Lembeni lililotabarukiwa na Askofu Rogath Kimaryo CSSP wa Jimbo Katoliki Same akishirikiana na Askofu Paul Semugerere wa Uganda. Balozi wa Vatikani nchini Askofu Mkuu Fransisko Padilla amepokelewa kwa shangwe na mwenyeji wake Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki Same pamoja na waamini wakiwepo mapadri, watawa na waamini walei. Akitabaruku Kanisa la Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi kigango cha Lomwe katika parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Usangi jimboni humo, Askofu Mkuu Padilla amewaasa waamini watambue wajibu wao kutegemeza Kanisa pamoja na paroko wao. “Mtambue kuwa, Kanisa la Mungu hapa Lomwe lina watu wenye uwezo mbalimbali wakimwemo wakulima, waajiriwa, wafanyabiashara ndogondogo na wafugaji. Hivyo lazima kujenga muungano wa sisi kwa sisi ili kusambaza injili ya Kristo katika eneo hili,” amesema Askofu Mkuu Padilla. Amesisitiza kujenga parokia katika msingi wa imani na hivyo kuwapokea wahitaji wa aina mbalimbali kiroho na kimwili. Aidha amesisitiza wanakanisa kusali na kuonesha matendo ya huruma kwa watu wote. Amewataka wajisikie furaha kulea miito ili siku moja kuwepo padri na watawa kutoka katika kigango hicho ili kushusha nyavu kuvua pamoja na Yesu. Amewataka waamini wajenge juhudi katika kuvua si wale tu wasiofahamu bali pia na wale walegevu na hivyo kuonesha sura ya Kristo kwa watu wote. “Tuogope kujihubiri wenyewe bali kumhubiri Kristo aliyekufa na kufufuka.” Balozi Padilla amekazia. Ameongeza “Ni vema kutafuta kondoo waliopotea tukiwapenda wote na kuwalinda huku tukiwapa tumaini la daima.” Askofu Mkuu Padilla amesisitiza kuwa jengo hilo liwe kweli nyumba ya sala na majadiliano ya kiroho. “Kwa kufungua na kubariki jengo hili basi mioyo ifunguliwe na kuguswa na Mungu. Kwa njia hiyo kuwepo mahusiano na masikilizano tukijua kuwa sote tu familia moja ya Mungu.” Ametoa mwito kwa wakristo kuwa na tabia ya kukubali mawazo ya wengine ili kuimarisha si idadi ya watu bali nguvu ya imani. Ili kufanikisha hayo, amewataka wote kujenga moyo wa kurithisha imani kwa watoto ili kuilinda na kuitetea kwa mapendo. Akistaajabu mandhari ya Lomwe Usangi, Askofu Mkuu Padilla amesema Wakristo katika eneo hilo lililopo katika milima ya upare wajivunie kwa vile wako juu karibu na mawingu hivyo, wako karibu na Mungu na Baraka za Mungu huwafikia kwa haraka. Wakati wa kutabaruku Kanisa hilo, Askofu Mkuu Padilla alibatiza watoto kumi waliokuwa wameandaliwa kama ishara maalum kwa utume wa Kristo wa kuwabatiza na kuwafundisha. Aidha ameongoza misa takatifu katika Kanisa Kuu la Kristo Mchungaji Mwema Same ambapo alitoa sakramenti ya kipaimara kwa waamini mia moja na ishirini na tano, na baadaye kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya mapadri na kubariki Groto ya Bikira Maria iliyopo katika uwanja wa Kanisa Kuu la Jimbo hilo. Pia ametembelea Parokia mama ya Jimbo ambayo ni Parokia ya Kilomeni na kubariki kikanisa cha masista. Hapo amewaasa wafurahi kwani kuwa juu ya milima ni kuwa karibu na mbingu na karibu na Mungu hivyo hupokea Baraka za Mungu kabla ya wengine. Katika adhimisho hilo walihudhuria pia Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya (Baba wa Mwanga), Mkuu wa Wilaya ya Same Herman Kapufi na wageni wengine kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo na serikali. Uongozi wa parokia umewashukuru wafadhili mbalimbali walioshiriki kujenga Kanisa hilo akiwemo Askofu Rogath Kimaryo, Paroko wa parokia hiyo Wilehard Mduma, Bw. Lameki Mlacha, Bw. Cassian Njowoka na wengine. Pia umewashukuru waliotoa eneo kwa uwanja wa Kanisa na pia kwa barabara ya kufika kanisani. Kutabaruku Kanisa Parokia ya Lembeni Akitabaruku Kanisa la Familia Takatifu Parokia ya Lembeni Jimboni Same, Askofu Rogath Kimaryo CSSP ametoa wito kwa waamini Wakatoliki kutunza majengo ya Kanisa ili yasiwe magofu bali kuonesha heshima ya pekee kwa Mungu ndani ya hekalu lake. “Tutunze nyumba ya Baba wala tusiichezee isije ikageuka gofu kwani kama tukiwa sisi tu wachovu wa imani jengo hili litakuwa kama gofu. Tusijaribu kupingana na hekalu la Bwana, yaani tusiwe kinyume, tusipinge Kanisa na daima tutambue kuwa Yesu ndiye silaha yetu. Sisi kama alivyokuwa Yesu tuwe na wivu na nyumba ya Baba,” amesema Askofu Rogath. Ameendelea, “Kutabaruku Kanisa hili kulete nguvu kwa njia ya Baraka ya Kanisa hili na tukwepe kuruhusu wachungaji wanaopitia madirishani, tuwakaribishe wote kwani wanapofika hawatarudi mikono mitupu kwani ni nyumba ya Mungu.” Amesisitiza kuwa, waamini ndiyo hekalu la Mungu yaani mawe yaliyo hai, hekalu la kweli na jiwe hai ambalo lilikataliwa na makandarasi lakini likawa jiwe kuu la pembeni. Kwa jinsi hiyo amewaasa wote walioshiriki waepukane na hali ya kutafuta kuangukiwa na jiwe hilo au kujikwaa katika jiwe hilo maana wakifanya hivyo hawatafaulu wala kupona. Aidha ameeleza jinsi waana wa Israeli walivyokaa uhamishoni Babeli na walivyorudishwa kwao kwa uongozi wa Nehemia aliyekuwa kiongozi aliyejaa unyenyekevu; na jinsi Nehemia alivyowataka watu wamjengee Mungu nyumba ya kuabudia kama utambulisho wao wakizingatia kuwa hekalu lilishabomolewa. Amesema kuwa siku hiyo ni siku ya Wanalembeni kufurahi na kumshukuru Mungu kwa makuu aliyowafanyia. Tusugue magoti yetu katika Kanisa hili kujiombea na kuombea wafadhili wetu ili neema za Mungu ziendelee kumiminika ndani mwetu. Askofu Rogath amewashukuru Mapadri hususani Paroko wa parokia hiyo padri Vicent Ndemchilio, wafadhili mbalimbali akiwemo Waziri Mstaafu Bw. Cleopa Msuya na Virani Mkomba kwa majitoleo yao ya kupenda maendeleo, na mshikamano bila kujali dini au dhehebu. Bw. Virani ameshirikisha yake ya moyoni akitanabaisha kuwa, kazi hiyo ilianza kwake kama njozi ambayo alimshirikisha mke wake na wazazi wake. Kwa nia njema wote waliafiki maono yake kuwa amjengee Mungu Kanisa. “Ieleweke kuwa thamani ya kujenga Kanisa ni kubwa na imegharimu vingi na kwa vile ni sadaka siyo majigambo itabaki siri moyo mwangu.” amesema Virani na kuendelea kuwa, “Ninawashukuru wafanyakazi wa kampuni ya VIGU kwa kufunga mkanda na kujitoa ili kufanikisha kazi hii ya kumpa Mungu heshima.” Parokia hiyo imejenga Kanisa jipya kuanzia April 13, 2013 na kutabarukiwa Mei 29, 2014, baada ya kuvunja Kanisa la zamani lililojengwa 1970.


IMG-20140603-WA0006

0 comments:

Post a Comment