MAKALA

Friday, June 6, 2014

imani za Freemason

ASKOFU Severine Niwe-Mugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, amekemea tabia iliyoanza kujitokeza katika siku za hivi karibuni ya baadhi ya watu hususani vijana, kuabudu mashetani kupitia Imani ya Freemason.
Ametoa kauli hiyo katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Dominika ya sita ya Pasaka ambapo vijana 250 wamepata Sakramenti ya Kipaimara. Ibada hiyo imefanyika katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu- Buseresere Askofu Niwe-Mugizi amebainisha kuwa ni aibu jamii ya sasa, hususani vijana kuamua kuishi kadiri watakavyo, wakidhan kuwa hakuna taratibu na miongozo ya Kanisa. “Wapo watu ambao wanapata mali kwa njia za kishirikina na hatimaye wanashangiliwa na jamii kwa ushindi walioupata,” amesema. Akizungumza kwa msisitizo, amesema jamii ya sasa imehalalisha maovu na wale wanaoyatenda wanashangiliwa. “Inashangaza kuona watu wanashangiliwa kwa maovu badala ya kushangiliwa kwa mema, hii siyo sahihi,” amesema. Imani ya kishetani Askofu Niwe-Mugizi ameendelea kueleza kuwa kadiri siku zinavyosonga, ndivyo vijana wanavyoendelea kuharibika. “Jamii ya sasa hushawishika kirahisi na kujiingiza katika tabia chafu na mbaya zaidi madawa ya kulevya na hatima wanajikuta wanatumbukia katika dimbwi la kuabudi mashetani (Freemason) ili wajipatie mali za haraka bila kutafakari madhara yake,” anasema Amewaasa vijana hao waliopata Sakramenti ya Kipaimara kuwa makini na mambo ya ulimwengu na kuepuka kudanganyika, kushawishika hasa kupenda mali zisizo za halali. Kuhusu siasa Katika hatua nyingine Askofu Niwe-Mugizi amegusia suala zima la Wakristo Wakatoliki kudharau masuala ya siasa na kufikiri kuwa wao siyo sehemu ya maisha hayo. “Mwaka huu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, baada ya chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu mwakani. Kuna tatizo la baadhi ya waamini kutoshiriki,” akasema Amekemea tabia ya baadhi ya waamini kubweteka na kutotimiza wajibu wao kihalali wa kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi wanaofaa bila kujali itikadi ya vyama vyao. “Tendo hili la mtu kutoenda kupiga kura ni dhambi ya kutotimiza wajibu,” amesema.

0 comments:

Post a Comment