MAKALA

Friday, June 6, 2014

Faida ya Maziwa ya Mama kwa mtoto

MTOTO anayezaliwa akiwa hai kitu cha kwanza anachokifanya ni kuvuta hewa. Baada ya hapo anaendelea na matendo mengine kama kulia, kucheka, kunyonya na mengineyo mengi anayoyafanya kadri umri wake unavyoongezeka. Mtoto huyo ili akue akiwa na afya iliyo bora anatakiwa kupewa maziwa ya mama ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza mtoto anyonye maziwa ya mama pekee hadi miezi sita ya kwanza bila kupewa chakula kingine chochote. Njia ya kawaida ya kupata maziwa ya mama ni ile ya mtoto kunyonya kutoka kwa mama yake mwenyewe au kukamuliwa maziwa hayo na kunyonyeshwa kupitia vifaa kama chupa, kikombe au kijiko kama kuna sababu la msingi. Mtoto mchanga anatakiwa kunyonya siyo chini ya mara kumi kwa siku. Mtoto huanza kupewa vyakula vya ziada kuanzia umri juu ya miezi sita ambapo maziwa ya mama huwa kama nyongeza hadi angalau miaka miwili na zaidi. Mtoto anaponyonyeshwa maziwa ya mama huwa katika hali nzuri zaidi kiafya na kuweza kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza endapo mtoto atakosa maziwa ya mama ikiwa ni pamoja na hatari ya kifo cha ghafla kwa mtoto mchanga. Licha ya mtoto pia mama anayekuwa ananyonyesha hupata faida nyingi akinyonyesha. Faida hizo ni pamoja na kurejesha uterasi katika hali yake ya kawaida na kupunguza kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua pamoja na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wingi wa maziwa ya mama hutegemeana mara ngapi mama hunyonyesha na/au kusukuma maziwa, mama anayenyonyesha mtoto wake zaidi au kukamua, ndivyo anavyotoa maziwa zaidi. Unyonyeshwaji wa mtoto unatakiwa kufuata matakwa ya mtoto wakati gani anataka kunyonya na siyo kufuata ratiba anayokuwa amepanga mzazi. Maziwa huanza kutoka baada ya kujifungua chini ya ushawishi wa homoni ambazo huchochewa zaidi mtoto anaponyonya mara baada ya kuzaliwa tu. Hii husaidia kulinda mtoto mchanga mpaka mfumo wa kinga yake unafanya kazi vizuri na inajenga athari ya kupumzika, huondoa mekoniamu na kusaidia kuzuia kujengwa upya kwa bilirubini (sababu muhimu ambayo huchangia ugonjwa wa macho kugeuka manjano). Maziwa ya mama ni chakula na kinywaji cha kwanza, na cha pekee kwa mtoto tangu kuzaliwa kwa hadi kufikia umri wa miezi sita. Maziwa ya mama ndiyo chakula bora kwa mtoto mchanga kuliko maziwa mengine au chakula kingine chochote ambacho anaweza kupewa mtoto. Mtoto anapofikia umri wa miezi sita anatakiwa kupewa vyakula vingine laini vya nyongeza huku akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi kufikia miaka miwili au zaidi. Umuhimu wa kunyonyesha Mama anayenyonyesha huweza kupunguza gharama ambazo angezitumia kununua maziwa au vyakula vya kumpatia mtoto.Gharama zinazotumika ni kidogo sana ambapo gharama hizo utumika kununua vyakula vya mama kula wakati wa kunyonyesha. Licha ya kupunguza gharama utafiti unaonyesha kuwa kuna manufaa mengi ambayo mama anayapata akimnyonyesha mtoto yakiwemo ya kuwa na afya bora, kupunguza uwezo wa kupatwa na baadhi ya saratani na manufaa mengine ya kisaikolojia. Mtoto anayekuwa anahitaji protini,mafuta,vitamini madini,homoni na virutubisho vingine muhimu ambavyo havipatikani sehemu vyingine iliyo sahihi tofauti na maziwa ya mama. Pia mtoto anaponyonyeshwa na mama anapata kinga mwilini mwake inayomkinga na maambukizi ya maradhi mbalimbali yanayoweza kumpata kama hatokuwa amenyonya maziwa ya mama. Mtoto anayenyonya maziwa ya mama anakuwa na kinga ya asili inayopatikana kwenye maziwa ya mama peke yake ambayo pia yanavirutubisho vyote. Mama anayemnyonyesha mtoto wake anakuwa na uhusiano mzuri kati yake na mtoto. Daktari huyo anasema kuwa mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama labda kama kuna tatizo la mama kufariki au sababu nyingine ambayo imedhibitishwa na daktari. Tofauti ya maziwa ya mama na mengine Maziwa ya mama yana tofauti na maziwa ya wanyama wengine wa aina ya mamalia. Maziwa ya mama yanakuwa tofauti na ya wanyama wengine kutokana na kila mnyama kuwa na tofauti katika muundo wa maziwa. Maziwa ya ng’ombe hayana vitamini E vya kutosha, chuma au asidi za mafuta muhimu kama yalivyo maziwa ya binadamu.Hali hiyo inaweza kusababisha upungufu wa damu kwa watoto wanaopewa maziwa ya ng’ombe. Matatizo yanayojitokeza wakati wa kunyonyesha Daktari Msaidizi wa Kituo cha Afya Kwenda Wilayani Karagwe, Dk Aristides Ruhikula anasema kuwa yapo baadhi ya matatizo yanayoweza kujitokeza wakati wa kunyonyesha ikiwa ni pamoja na mama kuvimba matiti yote au titi moja Sababu hii inaweza kujitokeza pale mama anaposhindwa kumnyonyesha mtoto wake ipasavyo ambapo hali hiyo inaweza kuendelea na kutoa jipu. Hali hiyo inatakiwa kudhibitiwa kwa kukamua maziwa ili kuyapunguza na kumyonyesha mtoto ili titi kurudi katika hali yake,hali hiyo haiathili ubora wa maziwa ya mama. Aidha mwanamke aliyechelewa kumnyonyesha mtoto mara baada ya kujifungua anaweza kuhisi kuwa hana maziwa hivyo anatakiwa amnyonyeshe mtoto wake ili kuweza kupata maziwa. Zaidi ya asilimia 98 ya wanawake huwanyonyesha watoto wao, na wengi wao huendelea kuwanyonyesha hadi kufikia umri wa miaka miwili au zaidi. Pamoja na jitihada za wanawake wengi kunyonyesha watoto wao, zipo kasoro zilizoanza kujitokeza kwa baadhi ya wanawake kukataa kuwanyonyesha watoto wao kwa sababu zao binafsi.Miongoni mwa sababu wanazozitoa ni pamoja na kuzeeka mapema watakapowanyonyesha watoto wao. Mama anayenyonyesha anatakiwa kuzingatia chakula anachokula.Mama huyu anatakiwa kula milo mitatu kila siku. Chakula hicho kinatakiwa kuwa mchanganyiko wa vyakula mbalimbali vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira anayoishi pamoja na mboga za majani na matunda pamoja na maji safi yaliyochemshwa. Ni muhimu jamii itambue umuhimu na kuzingatia lishe bora kwa mama anayenyonyesha. Pia mama huyo anatakiwa kupata muda wa kupumzika angalau dakika 30 kila siku mchana. Kwa wale wanawake wanaofanya kazi hivyo kulazimika kuwaacha watoto wao nyumbani kabla ya miezi sita Dk Ruhikula anashauri kuwa wanatakiwa kukamua maziwa yao na kuyahifadhi ili yatumike kwa ajili ya mtoto. Njia anayoshauri katika kuyahidhadhi ni kuyaweka katika chupa ya chai iliyo safi ili yaweze kubaki na joto lake linalohitajika tofauti na kuyaweka kwenye jokofu au sehemu nyingine ambazo zinaweza kupoteza joto lake.

0 comments:

Post a Comment